PROF. OLE GABRIEL AMKABIDHI OFISI DKT. JOHN JINGU, KATIBU MPYA WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amekabidhi rasmi ofisi kwa Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama na Katibu wa Tume Bw. John Antony Jingu

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika tarehe 22 Juni, 2026 katika ukumbi wa Tume jijini Dodoma ambapo pia watumishi wa Tume walipata nafasi ya kumuaga  rasmi Mtendaji Mkuu wa Mahakama Mstaafu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Prof. Ole Gabriel anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kumaliza vema majukumu aliyokabidhiwa na kufikia siku ya kumkabidhi ofisi Kiongozi aliyeteuliwa baada yake.

Aidha alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano. Aliongeza kuwa katika kipindi hicho, Rais Samia alimpa ushirikiano mkubwa na kuiwezesha Mahakama kufikia mageuzi makubwa.

Prof. Ole Gabriel pia aliwashukuru Viongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kumpatia ushirikiano na kumuelekeza wakati akitekeleza majukumu yake. Viongozi hao ni Pamoja na Jaji Mkuu wa TRanzania Mhe. George Masaju, Jaji Mkuu Mstaafu Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Siyani, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi aliyewahi kuwa Jaji Kiongozi Pamoja na viongozi wengine.

Kwa upande wa Tume ya Utumuishi wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel aliwashukuru Wajumbe wote wa Tume, Manaibu Makatibu na Watumishi wote wa Sekretariet ya Tume kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote alipokuwa Katibu wa Tume uliomuwezesha kuleta mafanikio makubwa kwa Tume.  

Aidha, aliwaasa Watumishi wa Tume kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya kazi zao ili kuhakikisha Tume inaendelea kupata mafanikio katika suala zima la utoaji haki kwa wananchi.

Kuhusu suala la kustaafu kazi kwa mujibu wa Sheria, Katibu huyo Mstaafu wa Tume aliwaasa Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuhakikisha wanaanza sasa kujiandaa na kustaafu na kutosubiri ibaki miaka michache au watakapotimiza miaka 60.

Alitoa wito kwa watumishi wa Tume kumpa ushirikiano wa kutosha na wa dhati Katibu Mpya wa Tume ili aweze kutekeleza vema majukumu yake mapya na kuendeleza yote mazuri yaliyopatikana wakati wa kipindi chake na pia aweze kuanzisha mambo mapya mazuri yatakayoiendeleza Tume na kuifikisha kwenye mafanikio makubwa zaidi.

Hafla ya makabidhiano hayo imekuja kufuatia aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Katibu wa Tume Prof. Elisante Ole Gabriel kustaafu kazi kwa mujibu wa Sheria na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kumteua Dkt. John Antony Jingu kuchukua nafasi yake.