JAJI KIONGOZI ATOA RAI JESHI LA POLISI KULINDA AMANI UTEKELEZAJI WA HUKUMU


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Geita

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani ametoa rai kwa jeshi la Polisi nchini kulinda amani na kuzuia uvunjifu wa amani wakati wa urtekelezaji wa amri halali za Mahakama.

Akizungumza na Wadau wa Utoaji haki hivi karibuni mkoani Geita wakati wa ziara ya Tume, Jaji Kiongozi alisema jeshi la Polisi pamoja na Viongozi wa Serikali wanayo nafasi kubwa katika kazi ya utoaji haki hususan kwenye mashauri ya madai.

”Polisi baada ya kujiridhisha juu ya uwepo wa amri halali za Mahakama, wanayo nafasi kubwa ya kusaidia kutunza amani”, alisema Jaji Kiongozi.

Alisema uzoefu katika maeneo mbalimbali nchini unaonesha kuwa jeshi la Polisi limeshindwa kusaidia kutoa ulinzi wakati wa utekelezaji wa amri za Mahakama hali inayoweza kuleta uvunjifu wa amani au amri za Mahakama kutotekelezwa.

Alisema kuna nyakati nyingine katika baadhi ya maeneo, Madalali wa Mahakama wamekuwa wakizuiwa na viongozi wa Serikali kutekeleza wajibu wao au viongozi hao kutoa amri kinzani na kuanzisha mchakato mwingine wa haki ikiwemo kusuluhisha baada ya amri ya Mahakama kuwa imeshatolewa.

Jaji Kiongozi alisema matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona Viongozi wa Serikali pamoja na Jeshi la Polisi, kama wadau muhimu wa Mahakama hawatakuwa vikwazo katika utekelezaji wa tuzo na amri za Mahakama. Aliongeza kuwa ikitokea kutoridhishwa na hukumu viongozi hao waelekeze kutumia fursa zilizopo kisheria kwa kukata rufaa.

Akizungumzia uanzishwaji wa Magereza, Mhe. Siyani alisema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kama mdau wa Mahakama haina budi kusogeza huduma hiyo ili kuziwezesha Mahakama za Mwanzo zilizo mbali na Magereza kufanya kazi kwa ufanisi na kurahishisha uhifadhi wa wafungwa na Mahabusu.

Alisema Serikali inao wajibu wa kuweka mazingira bora ya Mahabusu na wafungwa kama ambavyo kifungu cha 70 cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu  kinavyoitaka Wizara ya Mambo ya Ndani  kuanzisha Mahabusu ya wafungwa wanaohukumiwa na Mahakama za Mwanzo ili wapate hifadhi kabla ya kufikishwa mahakamani.

Akizungumzia ushiriki wa viongozi wa Serikali katika kujenga imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama, Jaji Kiongozi alisema mtaji wa Mahakama ni imani ya wananchi kwa kuwa wananchi wasipokuwa na imani hawataitumia Mahakama  na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani.

Alisema Sheria ya Usimamizi wa Mahakama namba 4 ya mwaka 2011 imewapa wakuu wa Mikoa na Wilaya nafasi ya kusimamia maadili ya Maafisa Mahakama ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.  Aliwataka Viongozi hao kutumia majukwaa mbalimbali waliyonayo kuifanya Mahakama iaaminike kwa wananchi.

”Mahakama inayoaminika ni msingi wa utulivu na amani katika nchi na amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya nchi”, alisema Mhe. Siyani.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imemaliza ziara ya siku nne ya kikazi katika mikoa ya Kagera na Geita yenye lengo la kujitangaza uwepo wake na kukutana na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mikoa na wilaya na wadau wa utoaji haki.