JAJI MANYANDA AWAAPISHA WAJUMBE WA KAMATI YA MAADILI WILAYA YA MLELE  


Na Mwandishi –Mahakama, Katavi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga, Mhe. Fedrick Manyanda amewataka wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kuzingatia maadili wanaposhughulikia malalamiko yanayowahusu Mahakimu.

Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Sumbawanga aliyasema hayo tarehe 19 Mei, 2025 alipokuwa akimuapisha Mkuu wa wilaya ya Mlele Bw. Majid Mwanga kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wa wilaya hiyo pamoja na wajumbe Kamati hiyo.              Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wajumbe hao, Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo alisema kuwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama hazina budi kutekeleza majukumu yake kwa Uadilifu na kwa kufanya hivyo itasaidia kuimarisha amani na usalama katika wilaya husika na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Manyanda pia aliikumbusha kamati kupitia tangazo la Serikali, tangazo Namba 1001 la mwaka 2020, na kuona jinsi lilivyo ainisha mienendo ya Maafisa Mahakama.

Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya ya Mlele inaundwa na Mhe. Majid Hemed Mwanga (Mkuu wa wilaya ya Mlele na Mwenyekiti wa Kamati), Bw. Yusuf  Mwenda (Katibu Tawala wa wilaya ambaye ni Katibu wa Kamati) Mhe. Lilian Moses Ndelwa (Mjumbe), Mhe. Nickson Temu (Mjumbe), Mhe. Fahamu Kibona (Mjumbe), Shekhe Awamu Kasoma (Mjumbe), Chief Michael  Mbogo (Mjumbe).

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

(Habari hii imehaririwa na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama)