JAJI MKUU AENDESHA KIKAO CHA MAKAMISHNA WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameongoza kikao cha Tume ya Utumishi wa Mahakama kilichojadili na kufanya Uamuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Uendeshaji wa Mahakama na Tume hiyo.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 9 Aprili, 2024 jijini Dar es salaam, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kikao hicho pamoja na mambo mengine, kilijadili na kutoa uamuzi juu ya kuajiri watumishi 112 wa Mahakama ya Tanzania wa Kada mbalimbali.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imefanikiwa kuendesha mchakato wa Ajira za Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa njia ya mfumo wa Kielekitroniki ambao umeongeza ufanisi, uwazi na kuwapunguzia gharama Wasailiwa wa nafasi mbalimbali za Ajira.

Katibu wa Tume alisema kikao hicho pia kiliwathibitisha kwenye vyeo viongozi walioteuliwa na kumudu vema madaraka waliyopewa pamoja na kuwathibitisha kazini watumishi wa kada mbalimbali. Aidha, Tume kama mamlaka ya nidhamu ilijadili na kutoa uamuzi juu ya mashauri ya nidhamu yaliyohusu watumishi wa Mahakama.

”Wajumbe wa Kikao hiki walipata wasaa wa kujadili taarifa za utekelezaji wa bajeti za Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi, 2024’’alisema Mtendaji Mkuu na Katibu wa Tume.

Akifafanua kuhusu Taarifa hizo, Prof. Ole Gabriel alisema, Tume kwa upande wake imeendelea na mikakati ya kuimarisha utendaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya pamoja na kuandaa Mwongozo na Kanuni za Uendeshaji wa Kamati hizo.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Tume unaoendelea jijini Dodoma, Prof. Ole Gabriel alisema hadi sasa umefikia asilimia 82. Jengo hilo la Tume lina thamani ya shilingi Bilioni 14.3

Akizungumzia  Taarifa ya Utekelezaji wa bajeti ya Mahakama ya Tanzania, Prof. Ole Gabriel alisema taarifa hiyo imeyataja baadhi ya mambo yaliyopewa kipaumbele na kushughulikiwa kuwa ni matumizi ya TEHAMA katika Usikilizaji wa mashauri, maboresho ya Sheria na Kanuni, maboresha ya upatikanaji wa kumbukumbu na taarifa kwa wakati, miundombinu ya majengo na teknolojia katika maeneo ya vijijini na mijini.

”Kuhusu maendeleo ya TEHAMA mahakamani, hadi kufikia Machi, 2024 Mahakama tayari imeanzisha Mifumo mbalimbali ya Kielektroniki ukiwemo ule wa wa Unukuzi na Tafsiri kwenye Mahakama 11 nchini pamoja na kuifanyia maboresho mifumo iliyopo”, alisema.

Alibainishwa kuwa Mahakama ya Tanzania  kwa kutumia Akili Mnemba (Artifial Intelligence) na mifumo mingine ya kisasa ya TEHAMA imekuwa kivutio kwa Mahakama duniani na sasa Viongozi wengi wa Mahakama za Afrika na Nje ya Afrika wanatembelea Mahakama ya Tanzania. Hii imewezesha pia utalii wa Mahakama (Judicial Tourism) na hivyo kuchangia pato la Taifa.

Kuhusu usikilizwaji wa mashauri mahakamani, alisema Tume ilipokea taarifa hiyo ambapo idadi ya mashauri ya mlundikano imeendelea kupungua kutoka asilimia sita mwaka 2021 na kufikia asilimia 3 Desemba mwaka 2023.

Alisema Serikali imeendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuiwezesha Mahakama kutekeleza majukumu yake pamoja na maboresho katika miundombinu yake.

Tume ya Utumishi wa Mahakama iliyoundwa na ibara ya 112(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika kutekeleza majukumu yake iliyopewa na Sheria, ilikutana katika kikao chake cha kawaida kwa ajili ya kujadili na kufanya uamuzi kuhusu masuala mbalimbali.

Pamoja na Mwenyekiti wa kikao hicho, wajumbe wengine waliohudhuria ni Mhe. Dkt. Gerald Ndika (Jaji wa Mahakama ya Rufani), Mhe. Mustapher Siyani (Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania), Jaji Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Bw. Bahame Tom Nyanduga (Wakili) na Bi. Dosca Mutabuzi (Wakili).  

Wengine waliohudhuria ni Prof. Elisante Ole Gabriel (Katibu wa Tume), Bi. Enziel Mtei (Naibu Katibu wa Tume-Ajira) na Bi. Alesia Mbuya (Naibu Katibu wa Tume-Maadili na Nidhamu). Aidha Mhe. Eva Nkya (Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania) alialikwa kuhudhuria kikao hicho.