JAJI MKUU ATAKA MASHAURI YATAKAYOTOKANA NA UCHAGUZI MKUU KUTOCHELEWESHWA
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Katavi
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji na Mahakimu kuwa na utayari wa kusikiliza mashauri yanayotokana na Uchaguzi na kutokuwa chanzo cha ucheleweshwaji wa uamuzi wa mashauri hayo.
Jaji Mkuu ameyasema hayo jana mjini Mpanda wakati akizungumza na Watumishi wa Mahakama katika ziara ya siku nne ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
”Huu ni mwaka wa uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, na kwa mujibu wa Katiba sisi Watumishi wa Mahakama hatutahusika na shughuli za kisiasa, tutahusika na kupiga kura tu”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema kutokana na uchaguzi huo kutakuwa na mashauri yatakayofunguliwa hivyo Majaji na Mahakimu wasiwe chanzo cha ucheleweshwaji wa mashauri hayo yanayotakiwa kuwa yamesikilizwa na kumalizwa ndani ya muda mfupi.
Jaji Mkuu alisema katika mchakato wa shughuli za uchaguzi Mahakama ya Tanzania imepewa majukumu kwa mujibu wa sheria hasa katika utatuzi wa migogoro inayotokana na uchaguzi huo. Aliongeza kuwa Sheria ya uchaguzi iliyotungwa mwaka jana inaonesha kuwa hata Mahakama za Mwanzo zina jukumu la kutatua baadhi ya migogoro ya uchaguzi.
Aidha, ametoa wito kwa Mahakimu na Naibu Wasajili kuisoma Sheria ya uchaguzi na kufahamu amepewa majukumu gani chini ya sheria ya hiyo ili mashauri ya uchaguzi yanapofika mbele yao waweze kuyasikiliza na kuyamaliza kwa haraka.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu wa Tanzania amewataka Watumishi wa Mahakama kuwa na tabia ya kutaka kujiendeleza kielimu kwa kuwa Dunia ya sasa inaihitaji mtu kujiongeza mwenyewe kujitafutia maarifa na ujuzi ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia.
Aidha amewapongeza Watumishi wa Mahakama mkoani Katavi kwa kutokuwa na mashauri ya Mlundikano ambapo alisema kuwa kukosekana kwa mshauri ya mlundikano ni dadlili kuwa watumishi wanafanya kazi kwa bidii na kutoa haki kwa wakati.
Akielezea malengo ya ziara ya Tume katika mkoa huo, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume alisema Tume imefika ili kuwakumbusha Watumishi hao Kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii na kiuchumi na pia kuwakumbusha umuhimu wa ushirikiano mzuri kati ya Mhimli wa Serikali na Mahakama.
Alisema alipozungumza na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko alimueleza kuwa kuna uhusiano mzuri kati ya Mahakama na Serikali mkoani humo na kila upande unaelewa mipaka yake.
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara ya siku nne katika mikoa ya Katavi na Rukwa yenye lengo la kuziimarisha Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za mikoa na wilaya ili ziweze kutekeleza ipasavyo jukumu lake la usimamizi wa maadili na nidhamu ya watumishi wa Mahakama.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.