JAJI MKUU AWAAPISHA MAKAMISHNA WAPYA WA TUME


  • Awataka kubuni utaratibu wa kupima utendaji kazi

Na Lydia Churi – Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaapisha Makamishna wapya wa Tume hiyo na kuwashauri kufikiria namna ya kuanzisha utaratibu wa kupima utendaji kazi wa mara kwa mara wa Watumishi wa Mahakama.

Jaji Mkuu ameyasema hayo mara baada ya kuwaapisha Makamishna wapya wa Tume hiyo katika hafla iliyofanyika leo tarehe 4 Machi, 2023 kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam. Makamishna hao waliteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kila mwaka Tume huajiri watumishi wapya na kuwapandisha vyeo wenye sifa lakini haijapata nafasi ya kupata taarifa za utendaji, ikiwemo kuchukua hatua kwa mtu aliyepewa nafasi ya kuwa Jaji, Hakimu, au Msajili anapokuwa ameshindwa au kiwango chake cha utendaji kimeshuka”, alisema.

Alisema kwa sasa Tume imejikita zaidi kwenye utovu wa maadili haijaangalia kwenye utoaji wa huduma, maeneo ambayo yanapaswa kuanza kufikiriwa ili kuwa na utaratibu wa kuangalia utendaji wa mara kwa mara kwa kila Mtumishi.

Aidha, Mwenyekiti wa Tume alimshukuru Rais wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha Tume ya Utumishi wa Mahakama na hasa kwa kuwahi kuteua Makamishna watatu ambao wamewezesha mwendelezo wa kufanya kazi za Tume bila kupumzika. “Tunamshukuru sana kwa kutupa Makamishna wenye historia zilizotukuka,” alisema.

Mwenyekiti huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru na kuwapongeza Makamishna wapya kwa kukubali utezi huo kwa kuwa jukumu walilopewa ni zito lakini pia aliwapongeza Makamishna waliomaliza muda wao wa kuhudumu katika Tume kwa kazi nzuri waliyofanya.

“Mnaweza kuona mchango wenu kwa kuangalia yale mafanikio tuliyofanya, idadi ya Majaji tuliyopendekeza kwa Rais na idadi ambayo ameikubali kuonyesha kwamba hatua za awali za mapendekezo zilifanyika vizuri. Nakumbuka hata idadi ya Mahakimu katika kipindi chenu ilikuwa kubwa sana. Kwa mwaka 2020/2021 tumeajiri takribani Mahakimu 200 au 300 na kuna masuala ya maadili mengi ambayo mmeyashughulikia,” alisema.

Aliwakumbusha Makamishna wapya kuzungumzia maslahi ya Watumishi wa Mahakama wanapotekeleza majukumu yao waliyopewa na kuzingatia maslahi ya wananchi kwa ujumla kwa kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi katika Tume. “Kazi yetu muhimu kama Tume ni kuangalia utumishi na utoaji wa huduma unaotolewa na Majaji na Mahakimu kwa niaba ya wananchi,” alisisitiza.

Kwa upande wao, Makamishna wapya kwa nyakati tofauti tofauti walimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwateua kushika nyadhifa hizo na kuahjidi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo vyao.

Makamishna waliomaliza muda nao wameshukuru kwa kuaminiwa kuitumikia Tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu. Aidha, Kamishna Mstaafu, Kalolo Bundala ameiomba Tume hiyo kuangalia uwezekano wa kutenga nafasi kadhaa za utumishi kwa ajili wa watu wenye mahitaji maalumu kama sera ya Serikali inavyoeleza.

Makamishna wapya walioapishwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald Ndika ambaye atatumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha pili. Wengine ni Wakili Msomi Bahame Tom Nyanduga na Wakili Msomi Dosca Mutabuzi. Makamishna waliomaliza muda wao ni Wakili Msomi Kalolo Bundala na Msomi Genoveva Kato.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Majukumu ya Tume yameelezwa kwenye Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. 

Aidha, wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais. Mtendaji Mkuu wa Mahakama  ndiye Katibu wa Tume hiyo.