JAJI MKUU AWAHIMIZA WANANCHI KUZIFAHAMU HAKI ZAO


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wananchi kuhakikisha wanafanya juhudi binafsi kuhakikisha wanazifahamu haki zao za msingi wao kabla ya kutafuta msaada wa kisheria.

Jaji Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 22 Januari, 2023 jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria iliyozinduliwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango baada ya kumalizika kwa matembezi yaliyoanzia kwenye kituo Jumuishi cha Utoaji haki Dodoma na kuishia kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini humo.

Alisema wananchi wanaotaka kutafuta haki, hatua ya mwanzo kabisa ni kuhakikisha wanafahamu wao wenyewe haki zao kwa kusoma au kutafuta elimu ya kuwawezesha kujua shughuli wanazofanya zinaongozwa na sheria ipi, kanuni na utaratibu upi”, alisema Jaji Mkuu.

‘Wananchi wakiwa kwenye ufahamu huo watakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupigania haki zao na kupata haki hiyo kwa urahisi”, alisema Jaji Mkuu.

Akifafanua kuhusu kauli mbiu ya Wiki ya Sheria kwa mwaka huu, Jaji Mkuu alisema inahimiza migogoro kumalizika haraka kwa njia ya usuluhishi. Alisema kuwa usuluhishi utawezekana pale tu ambapo Mahakama, wadau pamoja na wananchi wataona faida za kutumia njia hiyo katika kutatua migogoro.

“Katiba ya nchi inahimiza usuluhishi, inaitaka Mahakama inaposikiliza mashauri ya jinai Pamoja na yale ya madai ikuze na kuendeleza usuluhishi kwenye migogoro”. Alisema Jaji Mkuu.

Alisema utatuzi wa migogoro kwa kutumia njia ya usuluhishi una faida nyingi  ambayo ni pamoja na kutatua migogoro kwa muda mfupi na pia kwa gharama nafuu.

Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za Mahakama, Jaji Mkuu amewataka wananchi kutokubali kuachwa nyuma katika matumizi hayo kwani wakiachwa nyuma watapoteza ule ushindani na hivyo  kushindwa na wengine.

Maonesho ya Wiki ya Sheria yanafanyika jijini katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kuanzia leo na yatamalizika Januari 29, 2023. Aidha Siku ya Sheria nchini itakayofanyika tarehe 01 Februari, 2023 ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo ni Msimamizi wa shughuli za Mahakama ya Tanzania ni miongoni mwa Taasisi wadau wa utoaji haki nchini zinazoshiriki kwenye Maonesho hayo. Baadhi ya taasisi nyingine zinazoshiriki kwenye maonesho hayo ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Kurekebisha Sheria na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.