JAJI MKUU WA MAHAKAMA YA TANZANIA   NA MWENYEKITI WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA AMUAPISHA MHE.DKT. SAMIA NA MAKAMU WAKE


JAJI MKUU WA MAHAKAMA YA TANZANIA   NA  MWENYEKITI WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA AMUAPISHA MHE.DKT. SAMIA NA MAKAMU WAKE


Na Mwandishi Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amemuapisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Awamu ya Sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha pili.

Kadhalika, Mhe. Masaju amemuapisha Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hafla ya uapisho ilifanyika tarehe 03 Novemba, 2025 katika Uwanja wa Chamwino Ikulu jijini Dodoma na kushuhudiwa na wageni mbalimbali akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Marais na Viongozi kutoka Nchi mbalimbali za Afrika akiwemo Rais wa Burundi, Rais wa Zambia, Rais wa Msumbiji, Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia na kadhalika.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mabalozi kutoka Nchi mbalimbali, Viongozi wa Serikali, Bunge, Mahakama, Viongozi wa Dini na Wananchi kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya uapisho, Mhe. Dkt. Samia aliwasihi Watanzania kuendelea kulinda itikadi ya umoja, amani na mshikamano ambapo alisema, “ndugu zangu wote tunaoitakia mema Nchi hii ‘Tanzania’ tumesikitishwa na vitendo vya uvunjifu wa amani, upotefu wa maisha na uharibifu wa mali za umma na mali za watu binafsi kwenye baadhi ya maeneo hapa nchini hasa kwenye Majiji na Miji, kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania na sio Utanzania.”

Rais Samia alisema, Vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini vinaendelea kufuatilia na kuchunguza kwa undani zaidi kilichotokea na kuirudisha nchi katika hali iliyozoeleka kwa haraka.

Aidha, Mhe. Dkt. Samia alizitaka Kamati ya Kitaifa ya Ulinzi na Usalama na Kamati za Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuanzia jana tarehe (03 Novemba, 2025) maisha ya wananchi yanarejea katika hali ya kawaida mara moja.