JAJI MKUU WA TANZANIA ATEMBELEA MAONESHO YA SABASABA
- Asema Tanzania mahala sahihi kuwekeza, kufanya biashara
Na Faustine Kapama-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 5 Julai, 2024 ametembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 2024, maarufu Sabasaba, ili kujionea shughuli mbalimbali za uwekezaji na kiuchumi zinazofanywa na wananchi na Makampuni kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Mhe. Prof. Juma aliwasili katika Viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaam majira ya saa 5.00 asubuhi na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania na Mahakama.
Baada ya kupokea taarifa fupi kuhusu maonesho hayo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Bi. Ratifa Khamis, Jaji Mkuu alipitishwa katika Mabanda mbalimbali ambayo yalionekana kufurika wananchi.
Mhe. Prof. Juma aliongozwa na Mamlaka kutembelea mabanda tisa, ikiwemo Shirika la Bima la Taifa, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Wizara ya Viwanda na Biashara, Mahakama ya Tanzania, Magereza, Ofisi ya Waziri Mkuu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kutembelea Mabanda hayo, Jaji Mkuu amethibitisha ile Kauli Mbiu ya Maonesho ya 48, kwamba Tanzania ni mahala sahihi pa kufanya biashara na uwekezaji.
“Katika maeneo machache ambayo nimepata nafasi ya kuyatembelea nimeweza kuona uwekezaji mkubwa sana, hasa katika maeneo ambayo yatakuwa chachu kwa sekta binafsi kuweza kukua na kuendelea,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha kuwa yapo maeneo ambayo uwekezaji utasaidia huduma za biashara kuweza kufanyika, hivyo maonesho hayo yanatoa picha ya Tanzania ya sasa na ile inayokuja.
Amesema pia kuwa kuna maeneo mengine ambayo yanaweza kusaidia, hasa katika uwekezaji na biashara na kupunguza milolongo ya kutoa maamuzi.
“Siku hizi kuna dhana ya mchakato wa biashara (business process), tunaifanyia mchakato upya. Badala ya mchakato wa kibiashara kupitia hatua 10 au 20, tukiweza kuzipunguza kuwa hatua mbili au tatu, Tanzania itakuwa eneo bora la uwekezaji na biashara,” amesema.
Akizunguzia Banda la Mahakama, Mhe. Prof. Juma ameona uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali kama miundombinu ya majengo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na uwekezaji katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa na malalamiko yao yanafanyiwa kazi.
“Mahakamani kuna maboresho makubwa katika huduma, tumefikia hatua ya kutoa huduma ya Mahakama Inayotembea. Mahakama ni mfano katika matumizi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao unatumika pia katika kutoa haki…
“Wito wangu ni kwamba huduma za mtandao kadri zinavyosogezwa vijijini, hivyo hivyo huduma za Mahakama ndiyo zitazidi kusongea karibu na wananchi. Kwa hiyo ni uwekezaji mkubwa nimeuona,” Jaji Mkuu amesema.
Kabla ya Jaji Mkuu kuwasili katika Viwanja vya Sabasaba, Banda la Mahakama lilitembelewa na Majaji wa tatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Phocas Mkeha, ambaye ni Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Ubena John Agatho, Mhe. Dkt. Cleophace Morris na Mhe. Abdallah Halfan Gonzi.
Viongozi wengine waliotembelea banda la Mahakama ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas James Lyimo na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Wakili Msomi Harold Sungusia.