WATUMISHI WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA WASHIRIKI UFUNGAJI WA MICHEZO YA SHIMIWI KILIMANJARO


Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wameshiriki katika hafla ya ufungaji wa Michezo ya 40 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), iliyofanyika  Viwanja vya chuo cha Mafunzo ya Upolisi (CCP) Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Michezo hiyo iliyofanyika kuanzia tarehe 19 Septemba hadi 7 Oktoba 2026, imewakutanisha watumishi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwa na lengo la kuhamasisha ushiriki katika michezo, kuimarisha afya  pamoja na kujenga mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa umma.

Michezo hiyo iliendeshwa chini ya kauli mbiu “Watumishi wa Umma, Tupo Tayari kwa AFCON 2027,” inayolenga kuhamasisha watumishi wa umma kuwa sehemu ya maandalizi na hamasa kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yatakayofanyika kwa pamoja katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Hafla ya ufungaji wa michezo hiyo ilifanyika tarehe 7 Oktoba 2026, ambapo Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb)Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora  alikuwa Mgeni Rasmi. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa SHIMIWI, watumishi na washiriki wa michezo kutoka taasisi mbalimbali nchini.

Ushiriki wa Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama katika Michezo ya SHIMIWI unaonesha dhamira ya Tume ya kuhamasisha watumishi kushiriki katika shughuli za michezo kama sehemu ya kujenga afya bora, ustawi wa mtumishi na kuongeza ari na ufanisi katika utendaji wa kazi.

Aidha, michezo hiyo imekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha umoja, mshikamano, ushirikiano na mahusiano mema miongoni mwa watumishi wa umma kutoka taasisi mbalimbali, sambamba na kutoa fursa kwa watumishi kuonesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali.

Tume ya Utumishi wa Mahakama inaendelea kuunga mkono jitihada zinazolenga kuimarisha ustawi wa watumishi wake, ikitambua kuwa mtumishi mwenye afya njema na ustawi mzuri ana nafasi kubwa ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija katika kuwahudumia wananchi.