TUME YASHIRIKI KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA MKOANI PWANI


Tume ya Utumishi wa Mahakama ni miongoni mwa Taasisi za Serikali na wadau wa utoaji haki zinazoshiriki kwenye Kampeni ya Msaada kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili mkoani Pwani.

Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi jana tarehe 28 Oktoba, 2026 na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Abdallah Ulega katika viwanja vya Maili Moja Kibaha.

Tume inashiriki katika Kampeni hiyo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu majukumu yake pamoja na kushirikiana na wadau wengine wa utoaji haki kuelimisha wananchi kuhusu upatikanaji wa haki.

Kampeni hiyo yenye kauli mbiu ya “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo” inalenga kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu sheria pamoja na kuwasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria.

Huduma za kampeni hiyo katika Mkoa wa Pwani zinatarajiwa kutolewa kuanzia tarehe 29 Oktoba hadi 7 Novemba 2026, katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Tume ya Utumishi wa Mahakama inawahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo kupata elimu na kufahamu huduma zinazotolewa na Tume, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa wa umma kuhusu utumishi wa Mahakama na upatikanaji wa haki.