WATUMISHI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA MASJALA NDOGO YA MBEYA WATEMBELEA OFISI ZA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA


Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Mbeya wamefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama leo tarehe 27 Agosti, 2026 kwa lengo la kujifunza kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kiutumishi.

Ziara hiyo imewawezesha watumishi hao kupata fursa ya kufahamu kwa undani majukumu, shughuli na huduma zinazotekelezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama katika kusimamia masuala ya rasilimali watu ndani ya Mahakama.

Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Katibu wa Tume (Nidhamu na Maadili), Bi. Alesia Mbuya, aliwakaribisha watumishi hao na kuwapongeza kwa kutenga muda wa kutembelea Ofisi za Tume, hatua inayochangia kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya taasisi hizo.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Mtulya, aliongoza ujumbe wa watumishi waliotembelea Ofisi za Tume.

Pichani, mstari wa mbele katikati ni Naibu Katibu (Nidhamu na Maadili), Bi. Alesia Mbuya; kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, na kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi Tume ya Utumishi wa Mahakama Ndugu. Rickneville Mwanri, wakiwa pamoja na watumishi wa Mahakama Masjala ndogo ya Mbeya wakati wa ziara hiyo.