JAJI MTULYA AWAAPISHA WAJUMBE WA KAMATI ZA MAADILI YA MAAFISA MAHAKAMA
- Waelezwa majukumu yao
Na FRANCISCA SWAI, Mahakama – Musoma
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewaapisha Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya katika Mkoa wa Mara na kuwataka kuzingatia viapo vyao.
Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya walioapishwa jana tarehe 2 Julai, 2024 ni Wakuu wa wilaya za Musoma, Bunda, Tarime na Rorya ambao ni Wenyeviti wa kamati hizo pamoja na Makatibu Tawala wa wilaya hizo ambao ni Makatibu wa Kamati hizo. Aidha, wajumbe wengine wa Kamati hizo pia waliapishwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mtulya alisema kamati hizo zipo kwa mujibu wa sheria hivyo aliwataka wajumbe hao kuzingatia maadili ya viapo vyao na kutekeleza jukumu hilo la Kisheria kwa usiri na weledi mkubwa.
‘‘Sheria ya mienendo ya maadili ya Mahakimu inaeleza kwa undani hakimu aweje, aishije na namna ya kufanya kazi zake. Pale anapovunja sheria hizi au kukosea katika mwenendo wake ndipo kamati zenu zinafanya kazi,’’ alisema Mtulya.
Mhe. Mtulya aliwaasa wajumbe kuwa kazi zao si ndogo bali ni kubwa kwani wanatekeleza jukumu la kikatiba na kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji kamati hizi zinahusisha wajumbe wa namna mbalimbali ikiwemo wananchi wa kawaida, viongozi wa dini na viongozi wa kiserikali.
Aidha, Mhe. Mtulya amesisitiza wajumbe katika kutekeleza majukumu yao wakumbuke kuwa hawatekelezi majukumu hayo kwa vyeo vyao bali kama wawakilishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Katika zoezi hilo, wajumbe na viongozi wa kamati hizo walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali na kupewa ufafanuzi wa maswali yao. Pia walipewa elimu juu ya sheria mbalimbali zinazoelezea uwepo wa kamati hizo, namna wanavyoteuliwa, kazi za kamati husika, majukumu ya kila mjumbe katika kamati hizo pamoja na kuapa kwenda kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na weledi.
Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inahusisha wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.
Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
(Imehaririwa na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama)