KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA TUME KWA KUFANYA USAILI KIELEKITRONIKI  


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuendesha mchakato wa ajira za watumishi wa Mahakama kwa kutumia mfumo wa kielekitroniki na kuzishauri Taasisi nyingine zinazojihusisha na ajira kuiga mfano wa Tume hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 19 Aprili, 2023 jijini Dodoma wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo yaliyoandaliwa na Tume hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo wabunge hao kuhusu muundo na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama zikiwemo Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Edward Ole Lekaita alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama imepiga hatua kubwa katika suala zima la upatikanaji wa ajira hususan usaili kutokana na matumizi ya mfumo wa kielekitroniki ambao umesaidia kupunguza malalamiko kwa kiasi kikubwa.

Alisema kumekuwa na changamoto katika usaili na malalamiko yamekuwa ni mengi lakini endapo Taasisi nyingine nazo zitatumia mifumo ya kielekitroniki katika michakato ya ajira malalamiko yaliyopo yataisha.

Awali akizungumza, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel alisema Tume iliamua kutumia mfumo wa kielekitroniki kwenye mchakato ya ajira za watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kuendana na mabadiliko ya Teknolojia, kuongeza ufanisi na kutenda haki.

 

“Katika nafasi za ajira tilizokuwa nazo mwezi Juni, 2022, tulikuwa na nafasi 207 kwa kada mbalimbali, waliojitokeza kuomba nafasi hizo walikuwa ni zaidi ya watu 15,000, hivyo tuliona njia pekee itakayosaidia kutenda haki ni kutumia mfumo wa kielekitroniki ambao kwa kweli ulisaidia sana” alisema Prof. Ole Gabriel.  

Alisema Tume inaendelea kujiimarisha kwenye matumizi ya Tehama kwa kuongeza mifumo ya utendaji kazi ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023 kiasi cha  shilingi milioni 876 kimeombwa kwa ajili ya kusimika  mifumo ya ajira (Public Service Recruitment Portal) na nidhamu (Judicial Service Commission Ethics and Discipline Information System).

Kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya, Katibu wa Tume alisema kamati hizio zinasaidia kusimamia nidhamu na Maadili ya Watumishi wa Mahakama  na hivyo  kuboresha utendaji wa Maafisa  wa Mahakama katika ngazi zote.

Alisema Kamati hizo za Maadili ngazi za mikoa na wilaya wenyeviti wake ni wakuu wa mikoa na wilaya na zinaisaidia Tume katika kusimamia nidhamu na Maadili ya Mahakimu kwenye mikoa na wialaya husika hivyo wananchi wote wenye malalamiko yanayohusu nidhamu na maadili wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao kwenye kamati hizo.

”Nitumie nafasi hii kuwaomba wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kutusaidia kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati hizi ili waweze kuleta malalamiko yao dhidi ya ukiukwaji wa maadili”, alisema.

Prof. Ole Gabriel alisema ili wananchi waweze kufaidika na huduma zitolewazo na Mahakama katika kutoa haki, hawana budi kuelewa kazi za Tume ya Utumishi wa Mahakama, na zile za Kamati zake na umuhimu wa Tume katika kusimamia Mahakama ya Tanzania.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambaye ni Mbunge wa jimbo la Madaba Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuwafahamisha wabunge programu zake mbalimbali.

“Naipongeza sana Tume, mnaisaidia kamati kuifahamu Tume na kutekeleza majukumu yake vizuri na kwa viwango. Kila mnapopata fursa msiache kuitumia kutuelimisha kwa kuwa mnaisaidia Serikali, na pia Bunge katika kutekeleza jukumu lake”, alisema Dkt. Mhagama.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeandaa mafunzo kwa Kamati hiyo ya Bunge yenye lengo la kuelimisha na kuitangaza Tume hiyo. Mada ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Ilvin Mugeta ambaye alizungumzia muundo na majukumu ya Tume pamoja na mikakati mbalimbali ya kuimarisha utendaji kazi wa chombo hicho kinachosimamia utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania.

Katika Mada hiyo, Jaji Mugeta alisisitiza umuhimu wa viongozi kuwa makini na kauli zinazoweza kushusha heshima ya huduma zinazotolewa na Mahakama ili kujenga Imani ya wananchi kwa Mhimili huo. Alisema ni muhimu eneo la haki likazingatiwa kwa kuwa likivurugika nchi inaweza kuingia kwenye shida.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.