KAMISHNA NDIKA AZINDUA MFUMO WA KUTUNZA MAAMUZI YA KIMAHAKAMA


Na Mwandishi -Mahakama

Kamishina wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Gerald Ndika amezindua toleo la tatu la mfumo wa kutunza uamuzi wa kimahakama ujulikanao kama TanzLII ambapo hivi sasa utatumia pia lugha ya Kiswahili.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke Mkoa wa Dar es Salaam Kamishna huyo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alisema kuwa mfumo uliozinduliwa umefanyiwa uboreshaji ambapo hivi sasa utakuwa na uwezo wa kufanya kazi nyingi zaidi ikilinganishwa na ule wa awali.

“Natambua kuwa mfumo huu baada ya uboreshaji sasa una sura mpya na tutaanza kutumia toleo hili la mfumo unaotumia lugha mbili kwa maana ya Kiswahili na Kiingereza tofauti na awali ambapo ulitumia lugha ya kiingereza pekee”, alisema Mhe. Dkt. Ndika

Mhe. Dkt. Ndika aliongeza kuwa, mfumo huo sasa unamuonekano wa kuvutia sana, unaweza pia kupatikana kupitia simu janja ya kiganjani tofauti na ule mfumo ulipita ilikuwa sio rahisi kwa watumiaji kutumia kupitia simu ya mkononi.

Alisema hivi sasa mfumo wa TanzLii unaweza kupatikana kupitia simu janja ya kiganjani na pia ni rafiki kwa mtumiaji kwa kuwa unatoa fursa kwa mtu yeyote kuyafikia maamuzi ya kimahakama kwa njia nyepesi na unatoa matokeo sahihi zaidi.

“Mtafiti anayetafuta taarifa zinazohusu uamuzi wa kimahakama au sheria atapata matokea sahihi na kwa haraka kupitia mfumo huu ulioboreshwa, binafsi nimeshautumia”, aliserma Jaji Dkt. Ndika.

Jaji Dkt. Ndika alifafanua kuwa mfumo huo una sifa ya kipekee, ya kutumia kiungo maalum “hyperlink” inayomwezesha mtafiti kufanya kazi kutoka dirisha moja hadi jingine wakati wa utafiti. Mfumo uliopita haukuwa na kiunganishi hicho.

Alisema mfumo huo mpya utasaidia kuunganisha na kuboresha mahusiano ya Mahakama za kikanda kama vile Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariaki na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwenye eneo la maamuzi na sheria mbalimbali zilizotungwa. Aidha, mfumo huo hautaishia kwa wataalum wa sheria na watafiti pekee bali unalenga kumnufaisha mwananchi wa kawaidi ambaye atataka kupata nakala ya uamuzi ama sheria iliyokwisha pakiwa kwenye mfumo huo bila kutumia gharama, kuokoa muda na kumuondolea usumbufu.

Awali, akisoma histori fupi ya maendeleo ya matumizi ya mfumo wa TanzLII kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza alisema, ushirikianao na mahusiano mema baina ya Mahakama ya Tanzania na Chuo Kikuu cha Cape Town Afrika ya Kusini yamekuwa na tija kwa kuimarisha matumizi ya mfumo huo wa kutunza maamuzi ya kimahakama na kutengeneza namna bora ya ufikiaji na upatikanaji bure wa Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania kwa njia ya Mtandao.

Mhe. Kahyoza alisema kuwa, kwa kipindi chote Mahakama imeendelea kuchukua utaalamu na kupata uzoefu wa namna bora ya kuendesha na kuratibu maendeleo endelevu ya mfumo wa TanzLII hadi sasa unapoziduliwa toleo la tatu.

“Natambua jitihada za wadau wote SafLII, AfricnLII, Chuo Kikuu cha Cape Town Afrika ya Kusini na Mahakama ya Tanzania licha ya changamoto tumeendelea kushirikiana na tumeweza kuimarisha mfumo huu wa kutunza maamuzi yaani TanzLII”, alisema Jaji Kahyoza

Mhe. Kahyoza aliongeza kuwa, mfumo huo unawawezesha Majaji, Mahakimu, wanafunzi wa sheria wanataaluma ya sheria, mawakili na wananchi wa kawaida ufikiaji na upatikanaji bure wa maamuzi, sheria na kanuni za Tanzania kwa njia ya mtandao na kuifanya kuwa njia ya ufuatiliaji na usimamizi kwa viongozi wa Mahakama na ubora wa mfumo umethibitisha kuwa kiungo muhimu kwa utawala wa sheria nchini.

Sambamba na uzinduzi wa mfumo TanzLII, Mahakama ya Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Cape Town Afrika ya Kusini wenye lengo kuendeleza juhudi za kuboresha mfumo maalumu wa kutunza maamuzi ya kimahakama TanzLII na kutengeneza namna bora ya ufikiaji na upatikanaji bure wa Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania kwa njia ya Mtandao “TanzLII - Access Court Decisions and Laws of Tanzania for Free”.

Makubaliano hayo yalisainiwa tarehe 29 Mei, 2023 Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke jijini Dar es salaam kati ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Martin Chuma kwa upande wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mkurugenzi wa AfricanLII Bi. Mariya Badeva. Huku utiwaji saini huo ukishudiwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Kamishina wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Gerald Ndika.

Uzinduzi wa toleo la tatu la tovuti mpya ya Mfumo wa kutunza uamuzi wa kimahakama (TanzLII) ulihudhuriwa na machampioni wa mfumo huo, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Makatibu wa Sheria wa Majaji Pamoja na Wakutubi.