KAMISHNA NYANDUGA AIPONGEZA MAHAKAMA NA KUTOA RAI KWA TAASISI NYINGINE KUIGA MFANO


Na Mwandishi, Mahakama-Dodoma

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili Bahame Tom Nyanduga ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kupiga hatua katika uboreshaji wa huduma zake ikiwemo matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Akizungumza hivi karibuni jijini Dodoma katika kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Kamishna Nyanduga alisema kwamba, katika Sekta ya Sheria nchini Mahakama imepiga hatua kubwa Zaidi katika uboreshaji wa huduma za utoaji haki.

“Naomba nichukue nafasi hii kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa jitihada zake za dhati katika uboreshaji wa huduma za utoaji haki,” alisema.

Aidha, Kamishna huyo alitoa rai kwa Mhimili wa Mahakama kuyatangaza maboresho yake hata kwa Taasisi nyingine zilizo kwenye mnyororo wa utoaji haki ili nazo ziweze kwenda sambamba na kasi ya Mahakama katika uboreshaji huduma na hatimaye huduma ya utoaji haki nchini ipatikane kwa urahisi.

Miongoni mwa maboresho yaliyofanywa na Mahakama ni pamoja na kuongezeka kwa kasi ya uondoshaji wa mashauri kutoka asilimia 78 mwaka 2021 hadi kufikia 84 mwaka 2022, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo yake, kuongezeka kwa uwazi na uwajibikaji, uanzishwaji wa huduma ya Mahakama zinazotembea (Mobile Court services) na mengine.

Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kuwa kiwango cha umalizaji wa mashauri kimeongezeka kutoka asilimia 99 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 106 mwaka 2022. Aliongeza kuwa, hilo linaenda sambamba na kupungua kwa mlundikano wa mashauri kutoa asilimia 11 kwa mwaka 2021 na kufikia asilimia 6 kwa mwaka 2022 na asilimia 3 kwa mwaka huu.

Naye, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema Mahakama imepata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) sita na kuongeza kwamba, kwa sasa Mahakama ipo katika maandalizi ya awamu ya pili ya ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) tisa (9) pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Mahakama za Wilaya 15.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. 

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.