KAMISHNA WA TUME APONGEZA MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA KUIMARISHA UTOAJI HAKI


Na Mwandishi-Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amesema Mahakama ya Tanzania inapaswa kujivunia maboresho makubwa ikiwemo ujenzi wa mfumo mpya wa kielektroniki wa kuratibu mashauri kama sehemu ya kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), unaolega kuimarisha shughuli za utoaji haki.

Kaamishna huyo wa Tume ameyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwakaribisha Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kushiriki kwenye mafunzo ya siku mbili kuhusu mfumo mpya ulioboreshwa (Advanced e-case Management).

“Mahakama imekuwa kinara, inawezekana sisi wenyewe tupo humu ndani hatujifanyii tathmini na kutambua ni kwa kiasi gani tumepiga hatua katika matumizi ya TEHAMA, lakini tunaopata fursa ya kuwa na wadau wetu mbalimbali, ndani na nje ya nchi tunatambua hatua kubwa tuliyofikia,” alisema.

Alibainisha kuwa mfumo huo wa 'e-case management,' pamoja na mambo mengine, umekusudia kurahisisha kazi ya utoaji haki, ikiwemo kuwatoa kwenye kunukuu ushahidi na mienendo yote kwa mkono na kuwaleta katika mfumo wa kisasa ambao teknolojia itafanya kazi hiyo kwa niaba yao.

“Tunakoelekea ni kule ambako teknolojia itatumika zaidi kwenye kazi ya utoaji haki nchini, badala ya kumtegemea Jaji kuandika kila kitu kwa masaa mengi, kwanza kusikiliza, kutafsiri na kisha kuandika,” alisema huku akipongeza jitihada zilizofanywa na Kurugenzi ya TEHAMA na Usimamizi wa Mashauri na timu nzima inayoshughulikia masuala ya ujenzi wa mifumo kwa kukamilisha mfumo huo mpya.

Alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa mfumo huo, kwa hatua iliyopo hivi sasa, ni moja ya mafanikio makubwa ambayo Mahakama ya Tanzania inapaswa kujivunia inapopiga hatua kuelekea katika matumizi kamili ya TEHAMA kwenye utoaji haki.

“Tunaweza kufikiri kuwa ni kitu kidogo, lakini ujenzi wa mifumo siyo kitu chepesi, kutoa mawazo na kuyapeleka kuwa yenye kufaa kwenye akili bandia. Kwa asili ya kazi yetu inahitaji kuelewa ule mchakato wa kazi za Mahakama unafanyaje kazi na mchango wa wadau wetu,” amesema.

Alisema ni wazi mfumo wa 'e-case management' utasaidia kutatua changamoto na mapungufu mbalimbali ambayo yalikuwa yanakabili mifumo mingine iliyopita, ikiwemo JSDS2. Ametaja mambo machache ambayo mfumo huo utarahisisha shughuli za utoaji haki mahakamani tofauti na iliyokuwa kwa mifumo ya zamani.

Jaji Kiongozi amesema mfumo huo mpya utarahisisha ubebaji wa nyaraka, ikiwemo mienendo yote ya mashauri tofauti na JSDS2 ambao ulionekana kuwa umeelemewa na uzito wa nyaraka na ulikuwa hauhifadhi kumbukumbu za kutosha.

“Mfumo huu kwa sababu umeoanishwa na mifumo mingine, ikiwemo e-Wakili utasaidia kuwatambua Mawakili vishoka na pia kuondoa kadhia kubwa sana ambayo kila Jaji anaijua ya kupata kumbukumbu pale ambapo tunasikiliza rufaa au wakati wa kufanya mapitio,” amesema.

Mhe. Siyani alisema kuwa mfumo huo utarahisisha uitishwaji wa kumbukumbu kutoka kwenye Mahakama za chini ili kuwawezesha Majaji kufanya maamuzi, kwa maana utakapokuwa umetumika kwenye ngazi zote, mafaili yatapatikana kielektroniki kwa kutumia mfumo huo.

Alibainisha kuwa mfumo huo mpya utasaidia kuondokana na changamoto ya kupakia hukumu kwenye mifumo mingine ya kuhifadhia baada ya kumaliza kuandika na pia kuruhusu mienendo ya mashauri kuandikwa moja kwa moja na kurahisisha uandishi wa hukumu kupitia kiolezo maalumu na kisha kutuma moja kwa moja katika mfumo wa maktaba mtandao.

“Maboresho makubwa ya mfumo huu yamejikita zaidi katika kurahisisha usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao kupitia nyaraka pepe za kimahakama, upangaji wa mashauri kwa Majaji na Mahakimu, usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao pamoja na mambo mengi kadha wa kadha,” Jaji Kiongozi amesema.

Alisema kutakuwa na urahisi wa Mahakama kusomana na mifumo ya wadau wake muhimu, wakiwemo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wakala wa Usajili na Udhamini (RITA), Magereza, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), pamoja na wengine, hivyo kurahisisha kupata taarifa mbalimbali.