KATIBU WA TUME ATOA RAI KWA WADAU KUTUMIA TEHAMA KURAHISISHA UTOAJI HAKI


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa rai kwa wadau wa utoaji haki nchini kuendana na kasi ya Mahakama ya matumizi ya Tehama ili kurahisisha shughuli za utoaji haki na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda kwenye maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma, Katibu huyo wa Tume amesema wadau hawana budi kutambua kuwa Mahakama haiwezi kufanya kazi peke yake pasipo kushirikiana na wadau wake katika kutekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa watanzania.

”Mahakama ya Tanzania inataka kufika mbali, hivyo inatamani wadau wake waelewe kasi wanayokwenda nayo na wao wajitahidi kadri inavyowezekana kwenda nao sambamba, hususan katika masuala ya matumizi ya Tehama ili wawe na kasi moja ya kumhudumia mwananchi kwa ufanisi”, alisisitiza.

Alisema, Mahakama imefungua milango kwa wadau wake wote na itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, kwa urahisi na kwa gharama nafuu zaidi ili kumpunguzia Mwananchi mzigo.

Aidha, Katibu wa Tume anawaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyoandaliwa na Mahakama na kushirikisha wadau wake ili kupata elimu inayohusu masuala mbalimbali ya kisheria na haki kwa ujumla.

“Mahakama tumejiandaa kwa kiasi kikubwa na kwa kuzingatia mwongozo kutoka kwa Kiongozi wetu mkuu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, tupo tayari kuwahudumia wananchi na kuwaonyesha hatua kubwa ambazo tumefikia katika suala zima la utoaji haki nchini,” alisema.

Alisema kuwa ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria utafanyika tarehe 27 Januari, 2024 kwa kutanguliwa na matembezi yatakayoongozwa na Mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa maadhimisho hayo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson. Matembezi hayo yataanzia kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuishia katika Viwanja vya Nyerere Square. 

Maonesho hayo yanatarajiwa kumalizika tarehe 30 Januari, 2024 ambapo kilele cha Siku ya Sheria nchini kitafanyika tarehe 1 Februari, 2024. Mgeni rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Baadhi ya Taasisi zinazoshiriki kwenye maonesho hayo ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Takukuru, Mabaraza ya Ardhi, RITA na Tume ya Kurekebisha Sheria.

Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu 2024 inasema, “"Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai."