MAHAKAMA KUU KUANZISHWA MKOANI GEITA


Na Lydia Churi na Charles Ngusa-Geita

Mahakama ya Tanzania imeendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi ambapo hivi karibuni mkoa wa Geita utaanza kutoa huduma za Mahakama Kuu ambayo itakuwa ni  Mahakama Kuu ya mfano katika matumizi ya mtandao.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya za mkoani Geita, Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma amesema Geita itakuwa ni Mahakama Kuu ya kwanza kuachana na matumizi ya karatasi kwa kuwa itatumia zaidi mtandao kuendesha shughuli zake.

”Zaidi ya wananchi 2,977,608 wa Mkoa wa Geita wamekuwa wakienda umbali mrefu kufuata huduma huduma za Mahakama Kuu mkoani Mwanza, hivyo kuanzishwa kwa Mahakama Kuu katika mkoa huu kutasogeza karibu zaidi huduma kwa wananchi”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema maandalizi ya kuanzishwa kwa Mahakama Kuu mkoani Geita yanaendelea ambapo tayari jengo limefanyiwa ukarabati. Aliushukuru uongozi wa mkoa wa Geita kwa kuipatia Mahakama ya Tanzania jengo la muda litakalotumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ambayo majengo yake yatatumiwa na Mahakama Kuu.

Aidha, Jaji Mkuu alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigella kwa kuonesha utayari wa kuwa na huduma hiyo na pia juhudi kubwa ya kushirikiana na Mahakama  ili kuhakikisha mkoa wa Geita unakuwa na Mahakama Kuu.

Alimtaka Mkuu huyo wa mkoa kuendeleza juhudi zake katika kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo ni kuboresha hali ya maisha ya watanzania na ustawi wa wananchi wa mkoa wake na kuimarisha mazingira ya amani, usalama na umoja.   

Alisema Mahakama ya Tanzania inao mchango mkubwa katika uwepo wa mazingira ya amani, usalama na umoja kwa kuwa wananchi wanapofika mahakamani wanaamua kutatua migogoro yao kwa amani badala ya kutumia nguvu inayoweza kuvuruga amani na usalama wa nchi, hivyo kujenga utaifa na udugu.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewataka Viongozi na watumishi wa Mahakama mkoani Geita kujiandaa kuanzisha Mahakama Kuu hususan kuandaa mifumo ya Masjala.

”Mkuu wa mkoa wa Geita ameonesha uhitaji na utayari wa kuwa na huduma za Mahakama Kuu hivyo utayari wake ni lazima uendane na maandalizi mazuri”, alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amewataka watumishi wa Mahakama mkoani humo kutoa ushirikiano kwa Majaji,  viongozi wengine pamoja na watumishi watakaoanzisha masjala ya Mahakama Kuu.

Alimtaka Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzannia kuainisha mahitaji ya uanzishwaji wa Masjala hiyo pamoja na masjala nyingine za Mahakama Kuu zinazotarajiwa kuanzishwa kwa wingi hivi karibuni.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kasi yake katika uboreshaji wa huduma za kimahakama nchini na kuongeza imani ya wananchi kwa Mhimili huo. 

”Kila unapoona demokrasia inashamiri, amani na utulivu unaimarika ujue ni kwa sababu Mhimili unaosimamia haki unatimiza wajibu wake ipasavyo”, alisema Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa aliwataka wakuu wa wilaya ambao ni Wenyeviti ngazi ya wilaya kuona umuhimu wa kushirikiana na Mahakama katika kuimarisha utendaji kazi wa shughuli za utoaji haki mkoani Geita.

Aidha, Bw. Shigella alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Geita kutafuta kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Majaji.

Kuanzishwa kwa Mahakama Kuu mkoani Geita kutaifanya Mahakama ya Tanzania kuwa na jumla ya kanda 18 za Mahakama Kuu nchini. Lengo la Mahakama ni kuwa na Mahakama Kuu kwenye kila mkoa nchini. Mikoa ambayo bado haina huduma za Mahakama Kuu ni pamoja na Singida, Simiyu, Katavi, Lindi, Pwani, Songwe na Njombe.