MWENYEKITI WA TUME ASHAURI MATUMIZI YA USULUHISHI KATIKA KUTATUA MIGOGORO
Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewashauri wananchi wanaotafuta haki zao kutumia usuluhishi kama njia ya kutatua migogoro yao ya kisheria ili kuimarisha amani na ustawi wa jamii.
Akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu maadhimishio wa wiki na siku ya Sheria nchini jijini Dar es salaam, Mwenyekiti huyo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alisema Katiba ya nchi inawataka watanzania kujenga nchi inayozingatia misingi ya uhuru, haki na amani.
Jaji Mkuu alisema maadhimisho ya Wiki ya Sheria yatafanyika kitaifa kuanzia tarehe 22 hadi 29 Januari, 2023 katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma na yatatanguliwa na matembezi yatakayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango yatakayoanzia katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma na kuishia kwenye Viwanja vya Nyerere Square.
Alisema maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka huu itakuwa ni Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau ambapo Kilele cha maadhimisho haya ni siku ya Sheria nchini itakayofanyika siku ya Jumatano tarehe 01 Februari, 2023 katika viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma. Mgeni rasmi siku hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.
“Kauli mbiu inatoa ujumbe kuhusu wajibu wa Mahakama na wadau wake katika kutumia njia ya usuluhushi kutatua migogoro kwa lengo la kukuza uchumi endelevu, hivyo Wiki ya Sheria ni wakati Mahakama, wadau na wananchi watakumbushana na kuonyeshwa athari za kesi kuchelewa kukamilika kwa uchumi wa watu na wa nchi”, alisema Prof. Juma.
Alisema Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba inazungumzia kukuza na kuendeleza usuluhishi kama njia ya kutatua migogoro. Aliongeza kuwa njia hiyo mbadala ya kutatua migogoro inajumuisha utaratibu wa usuluhishi (Arbitration), upatanishi (Mediation), kurudisha mahusiano ya kirafiki (Reconciliation) na mazungumzo kufikia makubaliano (Negotiation).
Mwenyekiti wa Tume alifafanua kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ni takwa la Kikatiba na njia hii pia imehimizwa katika vitabu vya dini ambazo wengi wetu ni waumini wake. “Kwa hiyo, ni mpango wa Mwenyezi Mungu kuona watu wake wanatatua tofauti zao kwa njia ya usuluhishi”, alisema.
Aliosema utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, upatanishi, kurudisha uhusiano na mazungumzo una faida nyingi ikiwemo kupatikana haki kwa wakati na kwa gharama nafuu hivyo, kupunguza mlundikano wa mashauri mahakakani.
Alizitaja faida nyingine za kutumia usuluhishi kama njia ya kutatua migogoro kuwa ni kutumia muda mfupi kushughulikia migogoro na kubaki na muda mwingi zaidi wa kufanya shughuli za kiuchumi, kulinda mahusiano ya wadaawa kijamii na kiuchumi na kuhifadhi na kuendeleza mahusiano ya kibiashara na ya kijamii kwa wadaawa.
Akizungumzia matumizi ya njia ya usuluhishi katika nchi nyingine alisema kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika, nchi nyingi zilizoendelea, usuluhishi humaliza zaidi ya asilimia 90 ya migogoro inayofikishwa mahakamani. Alisema hali hiyo ni tofauti na Tanzania ambapo eneo hilo halipewi kipaumbele na Wadaawa na Wadau wa Mahakama kwa ujumla.
Alisema idadi ya mashauri yanayomalizika mahakamani kwa njia ya usuluhishi ni ndogo hali iliyosababisha Mahakama ya Tanzania kuja na kauli mbiu yenye lengo la kuhimiza utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Aidha, Jaji Mkuu amewahimiza wananchi wa mkoa wa Dodoma na maeneo ya Jirani kufika kwenye viwanja vya Nyerere Square ili wapate elimu kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi pamoja na masuala mengine ya kisheria.
Katika maonesho hayo, Mahakama ya Tanzania itatoa elimu pamoja na wadau wa Mahakama, wakiwemo Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).