MWENYEKITI WA TUME ASHIRIKI KUAGA MWILI WA CLEOPA DAVID MSUYA


Na Mwandishi-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwsenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameungana na Viongozi wa kitaifa na Watanzania kwa ujumla kuaga mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Cleopa David Msuya.

Jaji Mkuu aliungana na Viongozi wengine, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye maombolezo hayo yaliyofanyika kitaifa jana kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar-es-Salaam.

Miongoni mwa Viongozi wengine wa kitaifa waliomuaga Marehemu Msuya ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Aidha, Mwenyekiti wa Tume anatarajia kuungana na Viongozi mbalimbali wa kitaifa kwenye maziko ya Marehemu Msuya yatakayofanyika kesho tarehe 13 Mei, 2025 Usangi, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.

Mhe. Msuya alifariki tarehe 7 Mei, 2025 katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.

Kufuatia kifo hicho, Rais Samia alitangaza siku saba za maombolezo hadi tarehe 13 Mei, 2025 na kuwapa pole ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba huo mzito kwa Taifa.

Msuya aliwahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu mara mbili. Mara ya kwanza ni kuanzia tarehe 7 Novemba, 1980 hadi tarehe 24 Februari, 1983. Mara ya pili ilikuwa ni tarehe 5 Desemba, 1994 hadi tarehe 28 Novemba, 1995, huku akishika pia wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya kustaafu siasa aliendelea kushika nyadhifa kadhaa za uongozi katika Taasisi mbalimbali za Jamii.

Mhe. Cleopa David Msuya alizaliwa tarehe 4 Januari 1931 katika kijiji cha Chomvu, Usangi, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Makerere kuanzia mwaka 1952 hadi 1955. Baada ya hapo, alijihusisha na kazi za maendeleo ya jamii na huduma kwa Wananchi vijijini kuanzia mwaka 1956 hadi 1964.

Kuanzia mwaka 1964, Msuya alihudumu kama Katibu Mkuu katika Wizara mbalimbali: Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Utamaduni (1964–1965), Wizara ya Ardhi, Makazi na Maendeleo ya Maji (1965–1967), Wizara ya Mambo ya Uchumi na Mipango (1967–1970) na Wizara ya Fedha (1970–1972).

Mnamo tarehe 18 Februari 1972, Mhe. Msuya aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na alihudumu hadi alipohamishiwa kuwa Waziri wa Viwanda mnamo tarehe 3 Novemba 1975.

Baada ya kuhudumu kwa miaka mitano kama Waziri wa Viwanda, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mnamo Novemba 1980, nafasi aliyoshikilia hadi Februari 1983. Baadaye, alirudi tena kuwa Waziri wa Fedha kutoka Februari 1983 hadi Novemba 1985.

Tarehe 6 Novemba 1985, Mhe. Msuya alipewa jukumu jipya akiwa Waziri wa Fedha, Mambo ya Uchumi na Mipango hadi Machi 1989, kisha alirudi kuwa Waziri wa Fedha tena kuanzia Machi 1989 hadi Desemba 1990, na baadaye kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Machi 1990 hadi Desemba 1994.

Mwaka 1994, aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili, na pia kuhudumu kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi Novemba 1995.

Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Mhe. Msuya alichaguliwa tena kuwa Mbunge na alihudumu hadi alipostaafu rasmi tarehe 29 Oktoba 2000.

Baada ya kustaafu, Msuya aliendelea kuwa mwanachama hai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kufikia mwaka 2006 alikuwa bado ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Pia alikuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo la Kilimanjaro.

Mnamo Oktoba 23, 2019, akiwa na umri wa miaka 88, Mhe. Msuya aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo cha Ardhi.