MWENYEKITI WA TUME AWAPONGEZA WATUMISHI KWA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA UTOAJI HAKI


Na Mwandishi, Mahakama -Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza Watumishi wa Mahakama nchini kwa utekelezaji thabiti wa Mpango Mkakati na Programu za Maboresho zinazolenga kuboresha huduma za utoaji haki nchini.

Mhe. Prof. Juma alisema hayo tarehe 18 Mei, 2023 wakati akifungua Kikao cha siku mbili cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF jijini Dodoma.

“Kabla sijafungua kikao hiki muhimu, nitakosa fadhila na uungwana kama nitashindwa kuchukua nafasi hii kuwapongeza wafanyakazi kwa ufanisi ambao umejipambanua katika kufanikisha na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi,” amesema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu amesema ili kuendelea na maboresho ya huduma za Mahakama, Viongozi hawana budi kutambua nafasi na umuhimu wa Wafanyakazi, kwa kuwashirikisha kwa namna mbalimbali katika kupanga na kutekeleza kwa kadri ya uwezo wao. 

“Hapa madhumuni makubwa ni kuleta ufanisi na tija zaidi kazini na pia kuondoa migongano isiyo ya lazima, kuwashirikisha wafanyakazi ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanaelimishwa mara kwa mara kuhusu masuala yote muhimu ya Mhimili wa Mahakama yanayojitokeza kila siku,” amesema Mhe. Prof. Juma. 

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu alisema, rasimu ya taarifa ya REPOA ya utafiti kuhusu kuridhika kwa watumiaji wa huduma za Mahakama (Court User Satisfaction Survey) 2023 inaonesha kuwa kumekuwa na ongezeko thabiti la kiwango cha kuridhika na wepesi wa kuwasikiliza wateja , heshima na adabu inayoonyeshwa na wafanyakazi wa Mahakama kati ya mwaka 2015 na 2023.”

Akizungumzia safari ya maboresho ya Mahakama, Jaji Mkuu amesema TEHAMA imechangia kwa kiasi kikubwa huku akiendelea kusisitiza kuhusu matumizi ya Teknolojia kwa vitendo ili kutimiza azma ya kuwa na Mahakama mtandao (e-Judiciary).

“Ndugu Wajumbe na wageni waalikwa, naomba nitumie Baraza hili kutambua mchango mkubwa katika kuleta ufanisi uliotokana na matumizi ya TEHAMA. Nitumie pia Baraza hili kuendelea kukumbushana kuwa utoaji wa huduma kwa umma katika Karne ya 21 ni tofauti kabisa na ilivyokuwa miaka michache tu iliyopita,” ameeleza.

Kadhalika, Jaji Mkuu amesema watumishi wasiridhike na elimu na ujuzi walionao na badala yake kujiendeleza na kujisomea nje ya taaluma zao ili kuwa na uwezo wa kufanya kazi nyingi nje ya taaluma iliyowapa ajira (multi-task). 

“Jitihada binafsi za watumishi ndio zitaiwezesha Mahakama kuhimili pengo kubwa la idadi ya watumishi. Mahakama inahitaji watumishi 10,351, waliopo ni 6,000, sawa na asilimia 58. Karne ya 21 ni ya ubunifu. Kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa kuwa mbunifu na kuongeza thamani katika kazi anazofanya,” amesisitiza.

Amesema, Kikao cha Baraza, ni wakati mzuri wa kubadilishana uzoefu katika kukabiliana na changamoto, kukumbushana hatua iliyofikiwa tumefika na kujua wapi panahitaji kujirekebisha pamoja na kuwaelimisha watumishi kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa maslahi na haki zao.