RAIS SAMIA AMTEUA JAJI GEORGE MCHECHE MASAJU KUWA JAJI MKUU WA TANZANIA


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama

​​​​​​​Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 13 Juni, 2025 amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Kufuatia Uteuzi huo wa Rais Samia, Jaji George Masaju pia atakuwa ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 13 Juni, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka imeeleza kuwa, Mhe. Masaju anachukua nafasi ya Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye amestaafu.

Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, hafla ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu mteule itafanyika Jumapili tarehe 15 Juni, 2025 Ikulu-Chamwino mkoani Dodoma kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Mhe. Masaju alizaliwa tarehe 07 Aprili, 1965 katika Kijiji cha Bwai Wilaya ya Musoma mkoani Mara. Baada ya kuhitimu masomo katika ngazi mbalimbali za elimu ikiwemo Chuo Kikuu, aliajiriwa kuwa Wakili wa Serikali kuanzia mwezi Aprili, 1994 na kuendelea kufanya kazi hiyo hadi Oktoba, 2006.

Jaji Masaju amewahi kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini. Aidha, kuanzia mwaka 2006 hadi 2009, Mhe. Masaju aliteuliwa kuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Sheria na baadaye Oktoba, 2009 aliteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nafasi aliyohudumu hadi tarehe 02 Januari, 2015 alipoteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, tarehe 01 Februari, 2018, Mhe. Masaju aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na tarehe 20 Aprili, 2023, Mhe. Masaju aliteuliwa na Rais Samia kuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Sheria. Tarehe 10 Januari, 2025 Jaji Masaju aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Jaji Masaju anakuwa ni Jaji Mkuu wa Tanzania wa Saba Mzalendo na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama baada ya Jaji Mkuu wa Sita  Mzalendo Prof. Ibrahim Hamis Juma kustaafu kwa mujibu wa Sheria.