RAIS SAMIA APONGEZA UBORESHWAJI WA HUDUMA ZA MAHAKAMA


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kufanya uboreshaji wa huduma zake za utoaji haki na kutoa rai kwa Viongozi wa Mhimili huo kuhakikisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mahakama inazingatia ubora unaoendana na fedha zinazotolewa.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Sheria nchini yaliyofanyika tarehe 1 Februari, 2023 katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Rais Samia alisema amefurahishwa na uboreshaji wa miundombinu iliyosogeza karibu zaidi huduma za Mahakama kwa wananchi na kuwataka kutoa huduma zianazoendana na ubora wa miundombinu hiyo.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama kwa kuwezesha miradi hiyo ili kuweka mazingira wezeshi ya kufanyia kazi na kusaidia wananchi kupunguza gharama katika kutafuta haki mahakamani.

“Naipongeza Mahakama kwa maboresho mnayoendelea nayo toka mwaka 2015 pale mlipoamua kuandaa Mpango Mkakati wa Kwanza ambao umeleta mafanikio chanya,” alisema.

Rais Samia pia alipongeza Mhimili wa Mahakama kutokana mpango mzuri utakaosaidia kukamilika kwa taratibu za upatikanaji wa huduma za Mahakama Kuu katika Mikoa minane ya Singida, Pwani, Songwe, Katavi, Geita, Njombe, Simiyu na Lindi na mpango wa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika maeneno mengine, ikiwemo Pemba,” alisema.

Aidha, alipongeza uongozi wa Mahakama kwa matumizi mazuri ya fedha zilizotolewa na Serikali kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi wa majengo ya Mahakama.

“Natambua uwepo wa fedha kutoka Benki ya Dunia ambazo zimeimarisha miundombinu ya Mahakama, ikiwemo Mahakama za Mwanzo 60 na majengo mengine 18 ambapo kati ya hayo, 11 ni Mahakama za Wilaya na saba ni Mahakama za Mwanzo”, alisema.

Rais alisema Serikali yake itahakikisha kuwa taasisi zote zilizolko kwenye mnyororo wa utoaji haki, ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka zinapata pia miundombinu wezeshi ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Kuhusu usikilizwaji wa mashauri, Mhe. Dkt. Samia alipongeza kazi iliyofanyika huku akitolea mfano kwa mwaka 2022 ambapo Mahakama ilifunga mwaka ikiwa na mashauri 64,001, yakasajiliwa mengine 244,292 katika ngazi zote, hivyo kufanya mwaka huo kuwa na mashauri 304, 293, lakini yaliyomalizika yalikuwa 253,495.

“Ni kazi kubwa imefanyika, hongereni.  Nakubaliana nanyi kuwa kuongezeka kwa idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu toka 78 hadi 100 Agosti 2022 imekuwa chachu ya mafanikio hayo. Hili pia linachangiwa na dhamira ya dhati ya uongozi uliopo na Mahakimu wenyewe,” alisema.

Rais Samia alibainisha kuwa kwa sasa Majaji wamejielekeza kwenye utendaji wa haki na wanaendelea kutoa haki jinsi nafsi na sheria zinavyowatuma. “Hongereni sana Majaji, tunawashukuru sana. Naomba tuongeze kasi ili takwimu hizo zishuke lakini pia tujikite kuangalia ubora wa uamuzi unaotoka kwa kila shauri,” alisema.

Akizungumzia changamoto ya upungufu wa watumishi, Rais Samia alisema  kuwa Serikali itaendelea kufanyia kazi suala hilo la upungufu wa watumishi pamoja na maslahi na kuwahakikishia Majaji kuendelea kufanya kazi kwa bidi kwa kuwa  maslahi yao yataendelea kuboreshwa.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. El;iezer Feleshim katika salamu zake alisema kuanzishwa kwa Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi kutasaidia  kuwawezesha wadaawa na wanasheria kushughulikia migogoro na kuimaliza bila ya  kulazimika kwenda kwenye mabaraza ya nje.

“Umefika wakati wa kubadilisha Sheria ya Mwenendo wa Madai ili shauri la madai lipate sifa ya kusajiliwa mahakamani mara baada ya kupata uthibitisho kwamba zile ngazi za kupitia usuluhishi zimeshindikana.

Alimweleza Rais Samia kuwa ofisi yake na ile ya Wakili Mkuu wa Serikali wataendelea kusimamia vizuri matakwa ya sheria ya kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na kuendelea kusimamia kwa karibu maelekezo aliyoyatoa kuhusu jambo hilo ili kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa njia ya usuluhishi.

“Nitoe rai kwa Majaji na Mahakimu kuwa tayari kuwasilisha ofisini kwangu kwenye dawati linaloshughulikia utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali, kuhusu Wakili yoyote au mtendaji yoyote serikalini, ambaye kwa namna yoyote ile atathibitika kudhoofisha juhudi za Serikali na Mahakama za kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi,” alisema.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika Prof. Edward Hosea alisema kuwa chama chake kimeweka dhana ya Usuluhishi kwa vitendo kwa kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro Tanzania.

“Tunaamini kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria Kituo hiki kitaiweka Tanzania katika ramani ya Afrika na Dunia kwa kutekeleza dhana ya kutatua migogoro ya kibiashara za kimataifa na ile inayohusu wawekezaji kwa njia ya usuluhishi. Hatua hii itaimarisha kwa vitendo na kukuza mazingira rafiki kwa wawekezaji na wananchi wa Tanzania na kujenga imani katika mifumo ya utoaji haki na maendeleo,” alisema.

Baadhi ya viongozi wa Mahakama waliohudhuria Maadhimisho ya siku ya sheria nchini Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Katibu wa Tume, Prof. Elisante Ole Gabriel, Makamishna wa Tume, Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Wilbert Chuma na watumishi wengine.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Mawaziri wengine pamoja na Naibu Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wastaafu wa Mahakama na Serikali, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika,  watumishi wa Mahakama na wananchi mbalimbali.