RAIS SAMIA AWATAKA VIONGOZI KUTOKUWA CHANZO CHA MIGOGORO


Na Lydia Churi- Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi mbalimbali nchini kufanya kazi kwa bidii na kutokuwa chanzo cha migogoro katika jamii.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni wakiwemo Jaji wa Mahakama Kuu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Msajili wa Mahakama Kuu, Rais Samia aliwataka Viongozi hao kutumia nafasi walizonazo kutatua migogoro ya wananchi.

’’Kafanyeni kazi kwa ushirikiano baina yenu na mhakikishe mnawaunganisha wananchi badala ya ninyi kuwa chanzo cha migogoro kati ya wananchi”,   alisisitiza Rais Samia.

Viongozi wengine walioapishwa na Rais Samia jana Ikulu jijini Dar es salaam ni pamoja na Waziri na Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Naibu Makatibu wakuu wa Wizara mbalimbali.  

Awali akitoa salaam za Mahakama katika hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwataka Viongozi wa Mahakama ya Tanzania walioapishwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na kufuata misingi ya haki.

Akizungumzia nafasi ya Msajili Mkuu wa Mahakama, Jaji Mkuu alisema  Wasajili ni injini ya Mahakama ya Tanzania kwa kuwa wanalo jukumu la msingi la kusimamia suala zima la upatikanaji wa haki, hivyo alimtaka Msajili Mkuu aliyeapishwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili wananchi wapate haki kwa wakati.

”Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ni kiungo muhimu kati ya Mahakama, Serikali pamoja na Bunge” alifafanua Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu wa Tanzania alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kuongeza idadi ya watumishi wa Mahakama wakiwemo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Msajili Mkuu na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Alisema Mahakama ya Tanzania itaendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Mihimili mingine.     

Viongozi wa Mahakama walioteuliwa na Rais Samia tarehe 3 Aprili, 2024 kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Mhimili wa Mahakama ni Mhe. Sylvester Joseph Kainda aliyekuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Rais pia alimteua Mhe. Eva Kiaki Nkya kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Aidha, Rais alimteua Mhe. Chiganga Mashauri Tengwa aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita kuwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.