TUME YA UTUMISHI YA MAHAKAMA YAANZA ZIARA MIKOA YA KUSINI


Na Faustine Kapama– Mahakama, Mtwara

Tume ya Utumishi wa Mahakama chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Juni 20, 2022 ilifanya ziara ya siku tano kuzungumza na watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali katika mnyororo wa utoji haki na kutoa elimu kuhusu kazi zake katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Katika siku yake ya kwanza, Tume hiyo ambayo pia inajumuisha Makamishna na wajumbe wa Sekretarieti ilianza ziara yake kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti ambaye aliwakaribisha katika Mkoa wake na kuwahakikishia kuwa Serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mhimili wa Mahakama ili uweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Mkuu wa Mkoa huyo aliupongeza uongozi wa Mahakama kwa ujumla kwa uboreshaji wa huduma za utoaji haki kwa wananchi unaondelea ikiwemo kujenga miundombinu ya majengo ya kisasa pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), mabadiliko ambayo yamekuwa kichocheo kikubwa katika kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Alimweleza Mwenyekiti wa Tume hiyo pamoja na wajumbe wengine kuwa kwa muda wote tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa, hivyo kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili katika ngazi hiyo hajapokea malalamiko yoyote ya ukosefu wa maadili kwa watumishi wa ngazi zote za Mahakama.

“Mahusiano yetu na Mahakama ni mazuri sana, tunashirikiana (na) kuwasilina kwa karibu na Jaji Mfawidhi, tunatembeleana. Kwa kweli sina malalamiko, zaidi ya pongezi na nimwombe Jaji Mfawidhi kuwa ushirikiano tuliouanza uimarike zaidi na zaidi. Kwa niaba ya wenzangu, nipo tayari kuendelea kutoa ushirikiano unaohitajika kwa Mhimili wa Mahakama ili kazi zetu ziendelee vizuri,” alisema.

Baada ya ukaribisho huo, msafara wa Tume hiyo ulielekea katika Ukumbi wa Benki Kuu kukutana na watumishi wa Mahakama, Kanda ya Mtwara na kupokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Zainab Mruke na baadaye kufanya vikao na Wenyeviti wa Kamati za Maadili ngazi ya Mkoa na Wilaya na pia kuzungumza na wadau mbalimbali.

Katika taarifa yake ya utendaji, Mhe. Mruke amewaeleza wajumbe wa Tume hiyo, pamoja na mambo mengine, kuwa Mahakama ya Tanzania ipo katika uboreshaji wenye mikakati mbalimbali ya kupeleka huduma bora za utoaji wa haki na kuzifikisha karibu zaidi na wananchi kwa haraka zaidi.

Alisema kuwa viongozi na watumishi wa Mahakama wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kuwa azma ya utoaji huduma inayomlenga mwananchi inaendelezwa kwa nguvu zote, mafanikio ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na mabadiliko ya kifikra, maadili, kujiwekea malengo ya kazi na uwajibikaji.

“Kila mtumishi ametimiza wajibu wake kikamilifu kwa kufanya kazi kwa bidii na wakati mwingine zaidi ya masaa ya kazi bila manung’uniko. Kwa pamoja tutaifikisha Mahakama katika lengo kuu la Utoaji Haki kwa Wakati kwa Wote,” Mhe. Mruke amesema.

Akizungumzia suala la maadili katika Kanda yake, Jaji Mfawidhi huyo amebainisha kuwa katika Mwaka wa Fedha 2021/22 hakuna shauri lolote la uvunjifu wa maadili la watumishi wasio Mahakimu lililopokelewa na kuwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Watumishi wasio Mahakimu ya Kanda.

Alisisitiza kuwa maadili ya utumishi ni moja ya nyenzo muhimu katika kuwahudumia wananchi ambao ndiyo walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na Mahakama, hivyo usimamizi wake umekuwa ni kipaumbele namba moja katika usimamizi wa Rasilimali Watu. Mhe. Mruke amesema pia kuwa suala la maadili husisitizwa kila fursa inayopatikana kwenye vikao vya watumishi na hata vikao vya Menejimenti.

“Kukumbushana mara kwa mara wajibu wa watumishi wa miiko ya kimaadili ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vyovyote vya rushwa kumekuwa ni kinga muhimu katika kuwajenga kitabia na kimaadili watumishi wa Mahakama za Mkoa wa Mtwara,” amesema.

Tume ya Utumishi ya Mahakama imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Ibara ya 112 kwa lengo la kusimamia mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama. Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais. Mtendaji Mkuu wa Mahakama ndiye Katibu wa Tume hiyo.

Baadhi ya kazi za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya Majaji na kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.