VIONGOZI WA UMMA WATAKIWA KUTOINGILIA MCHAKATO UTEKELEZAJI WA HUKUMU


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Singida

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani ametoa rai kwa Viongozi wa Umma kutoingilia mchakato wa utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na Mahakama.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Tume na wadau wa utoaji haki uliofanyika jana mkoani Singida, Jaji Siyani alisema kumekuwa na matukio ya viongozi wa Umma wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya kuingilia au kuzuia utekelezaji wa amri na tuzo za Mahakama.

Alisema kuwa baadhi ya Viongozi hao wa Umma wamekuwa wakitaka hata amri za wito zinazotolewa na Mahakama zipitie kwenye ofisi zao, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa Mahakama.

“Kuzuia kwa namna yoyote utekelezaji wa amri za Mahakama ni kukiuka matakwa ya utawala bora”, alisisitiza Jaji Kiongozi.

Alisema endapo kuna mazingira yanayoashiria uhitaji wa kusimamisha utekelezaji wa amri za Mahakama, Viongozi wa Mahakama ngazi ya wilaya, mkoa na Mahakama Kuu wajulishwe na wahusika washauriwe kufuata utaratibu wa kisheria.

Alisema matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona viongozi wa Umma hawawi kikwazo katika mfumo wa utoaji haki na badala yake ushirikiano wenye tija uimarishwe na kuhakikisha waliotambuliwa na Mahakama kuwa wenye haki wanafaidi matumda ya haki zao.

Jaji Kiongozi pia aliwashauri wadau wa utoaji haki kujibidisha kufahamu vyombo mbalimbali vinavyohusika katika kutatua changamoto za wananchi ili kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa haki.

Wakati huo huo, Jaji Kiongozi amewataka wananchi kuondoa dhana ya kuwa hawawezi kupatiwa huduma mahakamani bila ya kutoa rushwa.

Alisema dhana hiyo ya rushwa iliyojengeka kwa miaka mingi haina budi kuondolewa kwa kuwa Mahakama hivi sasa inayo mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambayo imerahisisha kazi na kuleta uwazi katika suala zima la upatikanaji wa haki.

“Hatuwezi kusema rushwa imeondoka mahakamani kwa asilimia 100, lakini mifumo ya udhibiti iliyopo inatuthibitishia kuwa tuhuma nyingi za rushwa na ukosefu wa maadili zinazoelekezwa kwa Mahakama zinatokana na dhana”, alisema Jaji Siyani.

Alisema suala la tuhuma nyingi za rushwa kutokana na dhana au kutofahamika kwa taratibu ni jambo lililofanyiwa utafiti na tafiti zinaonesha wenye dhana hizi hawajawahi kufika mahakamani au hawajawahi kuwa na shauri mahakamani.

Jaji Kiongozi alisema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa Mhimili huu haukumbatii vitendo vya rushwa na badala yake watumie huduma za Mahakama bila hofu. Aliongeza kuwa matarajio ya Tume na Mahakama ni wananchi kama wadau muhimu wanaisemea Mahakama kwa uzuri ili kuiondoa dhana hiyo ya rushwa.          

Alisema dhana ya kuwepo kwa rushwa mahakamani itaondoka ikiwa wadau watashirikiana ipasavyo, maadili ya watumishi yatasimamiwa na mazuri yanayofanywa na Mahakama yatazungumzwa.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imemaliza ziara yake ya siku nne katika mikoa ya Dodoma na Singida iliyokuwa na lengo la kuitangaza Tume hiyo pamoja na kutoa elimu kwa watumishi, wajumbe wa kamati za Maadili ya Afisa wa Mahakama na wadau wa utoaji haki.