WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA WELEDI KATIKA KUELIMISHA WANANCHI KUHUSU TUME


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Waandishi wa habari wametakiwa kuzingatia weledi, nidhamu, uadilifu na uzalendo wanapotekeleza majukumu yao ya kuhabarisha na kuelimisha Umma kuhusu masuala yanayohusu utoaji haki hususan majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa Waandishi wa habari kuhusu Muundo na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma, Naibu Katibu wa Tume hiyo Bi. Enziel Mtei amesema ipo haja ya kutoa elimu kuhusu Tume ambayo moja ya majukumu yake ni kushughulikia malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili kwa Maafisa Mahakama ili wananchi waweze kuchukua hatua wanapokuwa na malalamiko. 

Naibu Katibu huyo aliwataka Waandishi wa habari wanaoshiriki mafunzo hayo kuisaidia Tume katika kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ikiwemo uwepo wa kamati za maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya ambazo hupokea  malalamiko ya wananchi yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa Mahakama.

”Zingatieni nidhamu, uadilifu na uzalendo kwa kutambua kuwa ninyi ni watanzania na siku zote mtangulize Taifa letu kwanza mnapotekeleza majukumu yenu ya kuhabarisha na kuelimisha Umma”, alisisitiza.

Alisema jukumu la Tume ya Utumishi wa Mahakama ni kuhakikisha Waandishi wa habari wanakuwa daraja muhimu kati ya Tume na wananchi kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu shughuli za Tume kwani ina matarajio ya kupata taarifa sahihi.

Bi. Mtei alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama itaimarisha na kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Waandishi wa habari kwa kwa lengo la kufikia hatua ya juu zaidi ya ufanisi katika uelimishaji na utoaji wa taarifa sahihi na muhimu kwa Umma.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya aliwataka Waandishi wa habari waliopata mafunzo kuhusu Tume kuwa mabalozi wa Tume kwa kuwaelimisha wananchi kuhusu Tume hiyo hususan uwepo wa kamati zinazopokea malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili kwa Maafisa Mahakama (Mahakimu) zilizopo kwenye ngazi za Mikoa na Wilaya ili waweze kuwasilisha malalamiko yao na kupata haki.

Awali akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa Mafunzo hayo, Afisa Habari Mwandamizi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Jonas Kamaleki alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama haina budi kuongeza kasi katika kujitangaza ili wananchi wengi zaidi waifahamu na kuitumia kwa kuwasilisha malalamiko yao.

Tume ya Utumishi wa Mahakama iliandaa mafunzo kwa Waandishi wa habari yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu muundo na majukumu yake ili washirikiane na Tume katika kufikisha elimu hiyo kwa wananchi wengi zaidi.