WAKUU WA MIKOA NA WILAYA WAOMBWA KUIKUMBUKA MAHAKAMA KATIKA MIPANGO YA MAENDELEO
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaomba wakuu wa mikoa na wilaya kuikumbuka Mahakama ya Tanzania katika mipango ya maendeleo hususan mpango wa kusogeza mkongo wa taifa wa Mawasiliano kwenye maeneo yao.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama katika mkoa wa Kigoma na wilaya zake leo Tarehe 20 Juni, 2023 mkoani humo, Mwenyekiti huyo wa Tume amesema kukosekana kwa mawasiliano ya mtandao kwenye majengo ya Mahakama husababisha shughuli za Mhimili huo kukwama kwa kuwa Mahakama ya sasa inatumia mifumo mbalimbali ya Tehama ili kurahisisha kazi ya utoaji haki.
“Majengo mapya ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini bado hayajaunganishwa kwenye mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, yatakapounganishwa yatasaidia mashauri kusikilizwa kwa haraka kwa njia ya Video”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ni wadau muhimu hivyo hawana budi kuielewa Mahakama inavyotekeleza jukumu lake la msingi la utoaji wa haki.
Alisema madhumuni ya Makamishna wa Tume kufanya ziara katika mikoa ya Kigoma na Tabora ni pamoja na kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili wa ngazi ya mkoa na wilaya. Aliongeza kuwa jukumu kubwa la wajumbe hao ni kusimamia nidhamu na maadili ya Maafisa Mahakama.
“Ninyi ni ramani inayotusaidia kuchora picha ya maadili kwa nchi nzima kupitia taarifa zenu mnazoziwasilisha kila miezi mitatu. Mnaiwakilisha Tume katika masuala ya nidhamu kwenye maeneo yenu”, alisema Prof. Juma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Bw. Thobias Andengenye alisema Serikali mkoani Kigoma itaendeleza ushirikiano wake na Mhimili wa Mahakama na kusaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizo ndani ya uwezo wake.
“Tutafanya kila tuwezalo kuilea Mahakama pasipo kuingilia uhuru wake ili tulinde heshima ya Mhimili huu muhimu”, alisema Mkuu wa Mkoa wa Kigoma
Akitoa neno la shukrani kabla ya kumalizika kwa Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa aliishukuru Mahakama kwa kusogeza huduma za utoaji haki mkoani Kigoma hususan kuanzisha na kujenga jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma pamoja na Mahakama nyingine za wilaya.
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wameanza ziara ya kikazi ya siku nne katika mikoa ya Kigoma na Tabora kwa lengo la kuitangaza Tume pamoja na kuziimarisha Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama.