WATUMISHI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA MATENDO YANAYOKIUKA MAADILI


Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Simiyu

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Gerald Ndika amewataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuepukana na matendo yote yanayokiuka Maadili ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya Mhimili wa Mahakama.

Akitoa mada kuhusu Muundo na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwenye Mkutano wa Tume na Watumishi wa Mahakama jana mkoani Simiyu, Jaji Ndika alisema Watumishi hao hawana budi kuepukana na matendo hayo kwa kuwa yatawaaibisha wao wenyewe na pia yatachafua taswira ya Mahakama.

“Tuzingatie pia kuwa jukumu tulilopewa la kutoa haki ni jukumu la kimungu na la kikatiba na ni muhimu sana katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu,” alisema Jaji Ndika.

Aidha, Jaji Ndika ametoa rai kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuzisoma, kuzielewa na kuzifuata kanuni za maadili ya watumishi wa Mahakama ili wafahamu haki zao na wajibu wao na kutoa huduma bora kwa wananchi. Alisema kuna changamoto ya watumishi kutofahamu haki na wajibu wao kwa kuwa hawasomi Sheria na kanuni za maadili.

‘Natoa rai kuwa ni vizuri kila mtumishi wa Mahakama asome kanuni za maadili na hasa kanuni ya 45 mpaka 75 kwani kanuni hizi ndizo zina utaratibu mpya wa usimamizi wa nidhamu. Utaratibu huu mpya ulianza kutumika Januari mwaka jana”, alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu uamuzi unaotolewa na Tume kwa watumishi wanaokiuka maadili, Dkt. Ndika alisema kwa upande wa Maafisa wa Mahakama/Mahakimu, uamuzi wa unaotolewa na Tume ni wa mwisho na hakuna rufaa. Alisema kwa watumishi wengine wa Mahakama wasio Maafisa wa Mahakama kama hawataridhika na uamuzi wa Tume wanayo nafasi ya kukata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma na ngazi yao ya mwisho ni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewataka watumishi wa Mahakama kuzisoma kanuni za maadili na kuzizingatia kwa kuwa ni kitu cha msingi katika maendeleo ya mtumishi yeyote wa Umma.

‘Nimesikitika sana kuona watumishi hawazifahamu kanuni za maadili, huu ni  ugonjwa ndani ya Utumishi wa Umma, usipopata nafasi ya kuaminika na kuteuliwa unaanza kuwalaumu viongozi wako unasahau kwamba ni lazima uzifahamu kanuni na kuzizingatia ili ufahamu haki na wajibu wako ” alisema Mwanasheria Mkuu.

Kuhusu kusimamia maadili, Kamishna Feleshi amewataka Mahakimu Wafawidhi kukutana na watumishi walio chini yao mara kwa mara na kuwajengea uwezo wa kimaadili ili kusaidia kuimarisha suala la maadili ndani ya Mhimili wa Mahakama.

Naye Kamishna wa Tume hiyo, Wakili Msomi Mhe. Genoveva Kato alihimiza watumishi wa Mahakama kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maadili mema kwani kwa kufanya hivyo watakuwa na nafasi kubwa ya kuendelea mbele zaidi katika utumishi.

Aidha, aliwataka watumishi wasio Maafisa wa Mahakama kutowakwaza Maafisa wa Mahakama wanapotekeleza wajibu wao bali wawasaidie na kuwawezesha ili wananchi wapate haki kwa wakati.

Kamishna Kato pia alimpongeza Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Shinyanga Mhe. Matuma Kirati kwa ubunifu wa kuunda kikosi maalum cha kushughulikia mlundikano wa mashauri na pia watumishi wa kanda hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya utoaji haki.

Kwa upande wake, Wakili Msomi Mhe. Kalolo Bundala amewataka watumishi wa Mahakama kujilinda siku zote na kujiepusha na mambo yote yaliyo kinyume na maadili mema ili kutoharibu taswira nzuri ya Mahakama.

“Kabla ya kutenda jambo lolote, jiulize je litaendeleza taswira nzuri ya Mhimili wa Mahakama?’. alisema Kamishna huyo.

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara katika mkoa wa Simiyu ambapo wamekutana na watumishi wa Mahakama pamoja na wajumbe wa Kamati za Maadili ngazi ya mkoa na wilaya.