WATUMISHI WA TUME WATAKIWA KUWA WAADILIFU NA WABUNIFU


Na Lydia Churi- Tume ya Uttumishi wa Mahakama-Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa na nidhamu, kufuata maadili na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa.

Akizindua na kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo leo tarehe 24 Aprili, 2023 jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria pia amewataka watumishi hao kuwa wabunifu wanapotekeleza majukumu yao ambayo ni pamoja na kuajiri, kusimamia nidhamu na maadili ya watumishi wa Mahakama na kumshauri Rais katika uteuzi wa viongozi wa Mahakama ya Tanzania.

“Suala la kuwa na nidhamu na maadili kwa watumishi wa Tume haliepukiki, huwezi kusimamia nidhamu kama wewe mwenyewe huna nidhamu na maadili mema”, alisema Dkt. Ndumbaro.

Alisema watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanapaswa kufanya kazi kwa ufanisi, kujituma na kuwa wabunifu kwani kumekuwa na changomoto kwa utumishi wa Umma kwenye suala la ubunifu. Aliongeza kuwa watumishi hao hawana budi kuwa wabunifu katika mchakato wa ajira, kusimamia nidhamu na maadili pamoja na kumshauri Rais katika teuzi mbalimbali za viongozi wa Mahakama.

Dkt. Ndumbaro alisema kazi na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ni ya kikatiba hivyo watumishi wake wanapaswa kuwa na nidhamu na heshima wakati wanapotekeleza majukumu hayo ya msingi.

“Ukiona umepewa majukumu ya kikatiba basi ujue heshima yako ni kubwa hivyo nanyi mnatakiwa kufanya kazi kwa heshima”, alisisitiza Waziri wa Katiba na Sheria.

Waziri wa Katiba na Sheria aliwataka watumishi hao kuwa waadilifu mara dufu katika matumizi ya fedha za Umma. Alisema kama Waziri hatafurahi kuona Tume hiyo ikionekana kwenye hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG).

Aidha, Waziri Ndumbaro aliwataka watumishi hao kutunza siri wanapotekeleza majukuimu yao kwa kuwa asili ya majukumu ya Tume ni siri. “Mchakato wa ajira ni siri, kusimamia nidhamu ni siri na kumshauri Rais katika masuala ya uteuzi wa viongozi ni suala linalohitaji siri”, alisisitiza.   

Aliwakumbusha watumishi kuwa mtumishi wa Umma popote duniani ni heshima na dhamana kubwa hivyo katika kuheshimu dhamana hiyo, wanapaswa kujituma na kuwahudumia wananchi wa Tanzania kwa haki na kwa usawa.

Akizungumzia uimarishwaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya mkoa na wilaya, ameitaka Tume kutoa kipaumbele kwenye bajeti ijayo katika kutoa elimu itakayosaidia usimamizi mzuri wa maadili katika ngazi za mkoa na wilaya.

Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watumishi wa Tume kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na kuwa wabunifu.

Alisema ni muhimu kwa watumishi kuwa na uelewa wa pamoja katika kazi na kuwa na mawasiliano ya karibu wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ili kuleta ufanisi kazini.  

Alisema viongozi hawana budi kuwathamini na kuwajali wale wanaowasaidia kutekeleza majukumu yao. “tushirikiane, tuheshimiane na tujaliane, tujenge utamaduni huo”, alisema Prof. Ole Gabriel.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.